Msamaha Poem by Fadhy Mtanga

Msamaha

Hakuna alokamilika, sote tuna mapungufu,
Hutokea kengeuka, kwani si wakamilifu,
Binadamu hupotoka, huonesha udhaifu,
Pale unapokosea, basi omba msamaha.

Usiogope kukosa, sote tumeumbwa hivyo,
Ni mtego tunanasa, vile tufikiriavyo,
Ama tukajenga visa, mengi t'watendeavyo,
Pale unapokosea, basi omba msamaha.

Wala sione aibu, kuuomba msamaha,
Mwenye kukosa hutubu, wala si kukosa raha,
Neno zuri ndo wajibu, kwa kuitunza staha,
Pale unapokosea, basi omba msamaha.

Samahani neno zuri, kwa wanaotuzunguka,
Tukosapo tukikiri, tunazidi heshimika,
Huo ndiyo ujasiri, tena usio na shaka,
Pale unapokosea, basi omba msamaha.

Haifai ujeuri, haifai endekeza,
Ijenge yako nadhari, watu itawapendeza,
Wala siyo jambo zuri, wenzako ukawakwaza,
Pale unapokosea, basi omba msamaha.

Makosa hurekebisha, zile tofauti zetu,
Msamaha huboresha, tuishivyo na wenzetu,
Upendo huimarisha, udugu kati ya watu,
Pale unapokosea, basi omba msamaha.

Hakuna aliye mwema, kwa asilimia mia,
Wenzetu wakitusema, haipaswi kuwanunia,
Makosa yanatupima, uwezo kuvumilia,
PALE UNAPOKOSEA, BASI OMBA MSAMAHA.

COMMENTS OF THE POEM
READ THIS POEM IN OTHER LANGUAGES
Fadhy Mtanga

Fadhy Mtanga

Dar es Salaam, Tanzania
Close
Error Success